Friday 29 July 2016

MO Bado Yupo Sana Msimbazi, Ataka Kufanya Uwekezaji Wa Bilioni 20


Tarehe July 29, 201610
Aliyewahi kuwa Mdhamini wa Klabu ya Simba, Bilionea Mohamed Dewji ‘MO’ amedai kuwa tatizo la klabu hiyo ni bajeti ndogo inayoifanya ishindwe kujipambanua vizuri mbele ya wapinzani wake wakuu, klabu za Yanga na Azam na kusema kuwa yupo tayari kufanya uwekezaji wa Shilingi bilioni 20 endapo wanachama wa klabu hiyo wataridhia.
MO ameyasema hayo leo katika kikao chake na waandishi wa habari na kudai kuwa kusuasua kwa klabu ya Simba kunachagizwa kwa kiasi kikubwa na ufinyu wa bajeti yake na kwamba kinachomvutia kufanya uwekezaji huo mkubwa kwa Simba ni mapenzi aliyonayo kwa klabu hiyo huku akijaaliwa kipato na Mwenyezi Mungu.
Amesema anaipenda Simba toka moyoni na kudai aliwahi kuidhamini miaka ya nyuma na kufanya vizuri sana katika michuano ya kimataifa na kila mwanamsimbazi anatambua hilo na kama atakubaliwa kufanya uwekezaji huo atajenga kiwanja bora cha mpira, hosteli, sehemu ya kufanyia mazoezi (gym), na kuajiri kocha mwenye viwango katika kipindi kifupi cha miaka mitatu tu.
“Tatizo ni bajeti na kutolea mfano bajeti ya Yanga akidai ni shilingi bilioni 2.5, Azam nao ni kiasi hicho hicho lakini kwa upande wa Simba hata nusu ya bajeti za wapinzani wao yaani shilingi bilioni 1.2 ni tatizo,” amesema.
Amefafanua kuwa ili klabu iweze kuleta ushindani mzuri ni lazima iwe na uwezo wa kununua wachezaji jambo ambalo limekuwa tatizo kwa klabu ya Simba.
“Ukitaka kushindana lazima uwe na uwezo wa kununua wachezaji lakini mnapotoa milioni 30 za usajili hatuwezi kushindana katika dirisha la usajili kwasababu wenzenu wanatoa zaidi ya hapo,” amefunguka.
Kauli hii ya MO inakuja huku zikiwa zimesalia siku chache tu klabu hiyo kufanya mkutano mkuu wa wananchama siku ya Jumapili katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay ambapo pamoja na mambo mengine suala la uendeshwaji wa klabu hiyo na uwekezaji unaotaka kufanywa na MO yatatawala katika mkutano huo

clouds stream