Tuesday 26 July 2016

Majaliwa Atoa Siku 14 Kupata Mpango Kazi Wa Kuhamia Dodoma

Tarehe July 27, 20161
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma siyo siasa kama watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili na kwamba Serikali inakamilisha eneo la kisheria juu ya uamuzi huo na kutoa siku 14 kwa uongozi wa Mkoa wa Dodoma kukamilisha mpango kazi na kumkabidhi mapendekezo.
Majaliwa amesema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Mkoa, Serikali za mitaa, viongozi wa dini, wajasiriamali, wazee wa mji huo, wasafirishaji, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi za elimu, za kifedha na watoa huduma mbalimbali katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina ndogo Mjini Dodoma.
Amesema hapa tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa pamoja na hakuna namna nyingine kwa sababu uamuzi umeshatolewa na kuwahakikishia kwamba suala hilo sio la kisiasa kwani kinachokamilishwa sasa ni eneo dogo tu la kisheria juu ya uhamishaji wa makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii itapitishwa.
Waziri mkuu ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake wakae na kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ndani ya siku 14 mkoa na kumkabidhi mapendekezo yao ili yaweze kuingizwa kwenye mpango mkubwa wa Serikali kuu.
“Uongozi wa Mkoa, ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais TAMISEMI usimamie na kuyaratibu majukumu haya na ndani ya siku 14 nipate mapendekezo (proposal) ya kwanza na namna mtakavyoyatekeleza,” amesisitiza.
Amesema chimbuko la uamuzi wa kuhamia Dodoma na kuifanya kuwa Makao Makuu ya Serikali lilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo imeendelea kudumu katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 chini ya Ibara ya 151. 
“Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na viongozi wengine wote wa Chama kwa kusimamia ndoto ya Baba wa Taifa ya kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa wananchi wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa ujumla, amesema.

clouds stream