Wednesday 20 July 2016

Serikali Kununua Rada Mbili Kusaidia Ukusanyaji Wa Mapato


Tarehe July 20, 2016Radar-hatzerim-1-1
Radar-hatzerim-1-1
Serikali imetangaza kununua rada mbili mpya kwa ajili ya kusaidia kukusanya mapato zaidi ya Shilingi bilioni 18 ambazo zinapotea kila mwaka kutokana na kukosekana udhibiti katika anga la Tanzania.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Teknolojia, Edwin Ngonyani,  amesema hayo katika mkutano uliowakutanisha wataalamu wa masuala ya anga pamoja na wamiliki wa kampuni za ndege barani Afrika.
Amesema katika awamu ya kwanza, Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kununua rada mbili ambazo zitafungwa kwenye viwanja vya ndege vya Mwalimu Julius Nyerere na Kilimanjaro (KIA), huku awamu ya pili ikifungwa katika viwanja vya Mwanza na Songwe.
“Serikali tayari imeshatenga bajeti kwa ajili ya kuhakikisha kuwa inanunua rada mbili, ili kuokoa kiasi cha takribani shilingi bilioni 18 ambazo zimekuwa zikipotea kila mwaka, jambo ambalo linafanya nchi kupoteza mapato, kwani inakuwa haiwezi kulisimamia anga lake lote na hivyo kufanya ndege, hata zile zisizotua nchini huku zikitumia anga hilo, kushindwa kulipa ushuru,” amesema.
Kwa sasa Kenya na Rwanda ndiyo nchi zenye rada hizo licha ya kuwa nchi hizo ni ndogo ukilinganisha na Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurungezi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TCAA), Hamza Johari, amesema kuwa ununuzi wa rada hizo utasaidia kuongeza mapato na hivyo kufanya viwanja vya ndege kujiendesha vyenyewe bila kusubiri msaada kutoka serikalini.
Mkutano huo ulikuwa ukikutanisha wamiliki wa ndege zilizokidhi vigezo na wadau mbalimbali wa masuala ya anga kutoka Bara la Afrika, ukiwa na lengo la kujadili changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.

clouds stream