Tuesday 26 July 2016

Sumatra Yafungua Makucha,Yafutia Leseni Madereva Na Mabasi


Tarehe July 26, 2016Baadhi ya mabasi ya mikoani katika moja ya kituo cha mabasi nchini.
Baadhi ya mabasi ya mikoani katika moja ya kituo cha mabasi nchini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesitisha leseni za madereva 18 kutokana na mgomo walioufanya kupinga wenzao kupelekwa mahakamani.
Aidha,Wamiliki wa mabasi 12 ambayo madereva hao walikuwa wanaendesha kwenda sehemu mbalimbali nchini, wamepewa siku saba kujieleza ni kwa nini wasifutiwe leseni za kutolea huduma hizo pamoja na kutakiwa kusitisha ajira kwa madereva hao.
Kwa mujibu wa  Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alisema Julai 23 mwaka huu mkoani Kagera, madereva wa mabasi hayo walifanya mgomo kupinga kitendo cha madereva wenzao kupelekwa mahakamani, kukosa dhamana na kulala rumande kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwamo kuendesha kwa mwendo kasi.
Kamanda Mpinga alisema dereva yeyote atakayeendesha gari kwa kasi ya zaidi ya kilometa 90 kwa saa atafikishwa mahakamani na sio kutozwa faini kama awali ili kuhakikisha matukio ya ajali yanapungua nchini.
Alisema kutokana na hali hiyo madereva wanaoendesha mabasi yanayoanza safari zake kwenye Manispaa ya Bukoba, walisitisha huduma kwa kushinikiza Mahakama iwaachie wenzao waliokamatwa kwa makosa ya mwendo kasi.
Naye Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe, aliyataja mabasi pamoja na madereva waliositishiwa leseni kuwa ni Hussein Tegatega na Miraji Kondo wa Kampuni ya RS Express wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 425 DDT aina ya Zongtong linalotoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Said Omary na Amos Danney wa basi la Kimotico lenye namba za usajili T 966 CDY aina ya Nissan linalotoka Bukoba kwenda Arusha na madereva wanne wa mabasi ya Princess Muro yenye namba za usajili T 166 DCA na T 923 DCT yanayosafiri kutoka Bukoba kwenda Dar es Salaam.
Madereva hao ni Ally Mshuza, Twalibu Ondossy, Costa Andrew na Witness Lema.
Wengine  ni Musa Tindwa na Gerald Beti wa Kampuni ya Osaka Raha wanaoendesha basi lenye namba za usajili T 968 CPC linalofanya safari zake Bukoba kwenda Dar es Salaam na Paul Ngussa wa basi lenye namba za usajili T 810 BDW aina ya Scania linalotoka Bukoba kwenda Musoma, mali ya Kampuni ya Bunda Express.

clouds stream