Monday 4 July 2016

Mabasi Ya Mwendokasi Kuanza Kutumia Gesi


Tarehe July 4, 2016dart
dart
Msimamizi wa Usambazaji Gesi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Ismail Naleja, amesema awamu ya pili ya mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam yatatumia nishati ya gesi asilia badala ya mafuta jambo litakalosaidia kupunguza gharama.
Akizungumza katika Maonesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Naleja alisema hatua hiyo itaongeza idadi ya magari yanayotumia gesi nchini ambapo hivi sasa kuna mabasi 60 yanayotumia gesi na kuwashauri wenye magari kutumia mfumo huo ili kupunguza gharama za uendeshaji.
“Uendeshaji wa gesi utakuwa nafuu jambo linaloweza kufanya hata nauli zake kupungua kwani kilo moja ya gesi inatumika katika umbali unaotumiwa na mafuta ya dizeli lita moja na nusu,” alieleza Naleja.
Alisema kilo moja ya gesi ni Sh 1,500 wakati lita moja na nusu ni Sh 3,000, pia gesi haiharibu mazingira kwa sababu haina kaboni ikilinganishwa na petroli.

Mtaalamu huyo alisema matumizi ya gesi katika magari si hatari, kwani gesi inayotumika ni nyepesi kuliko inayotumika majumbani, hivyo ikivuja inasambaa hewani na tatizo likitokea mtungi wa gesi unajifunga.

clouds stream