Thursday 7 July 2016

Shein Asisitiza Hakuna Serikali Ya Mpito, Maalim Akidai Yupo Tayari Kukamatwa


Tarehe July 7, 2016Shein
Shein
Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi mkuu visiwani humo ulishamalizika na hakuna mpango wa kuwepo kwa serikali ya mpito.
Rais Dkt. Shein ameyasema hayo jana katika Baraza la Idd na kudai kuwa uchaguzi mwingine utafanyika mwaka 2020 na kuahidi kupambana na wale wote wanaoihujumu Serikali yake kwa namna moja ama nyingine ishindwe kutekeleza mipango yake ya maendeleo.
Amesema wapo watu wamekuwa wakijaribu kufanya mbinu na vituko serikali ishindwe kutekeleza mipango yake, ikiwemo kusimamia ilani ya chama na bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/2017.
“Wananchi napenda kusema tena kwamba uchaguzi umekwisha na utafanyika mwingine ifikapo mwaka 2020…wanaotaka kuwepo kwa serikali ya mpito wasahau,” amesema.
Amesema hakuna sababu ya kuwepo kwa serikali ya mpito kwa sababu CCM ilishiriki katika uchaguzi wa marudio na kushinda kwa kishindo na kuwataka wananchi kupuuza propaganda zinazotolewa na wapinzani kwa ajili ya kile alichosema ni kuwazubaisha wananchi washindwe kufanya kazi zao vizuri.
Rais Shein pia amekemea matukio ya uvunjifu wa amani yanayojitokeza zaidi katika kisiwa cha Pemba na kuvitaka vyama vya siasa kufanya kazi zao bila ya kukiuka sheria zilizopo kwani vitendo vya chuki na ufisadi ni kinyume na maagizo ya Mungu.
Kauli hii ya Rais Dkt. Shein inazidi kufifisha tumaini la wapinzani wakuu Chama Cha Wananchi CUF, ambao wamekuwa wakihaha tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio Machi, mwaka huu visiwani huko wakidai kuwa uchaguzi huo ulikuwa haramu na hawautambui huku wakitoa wito kwa uchaguzi mwingine kufanyika.
Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amesema Jeshi la Polisi kama lina nia ya kumkamata na kumweka ndani lifanye hivyo kwa kuwa yeye yupo nchini.
Maalim Seif ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Wakfii wa Ngazija mjini Zanzibar, tofauti na jingine lililofanyika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani na kuhutubiwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Amesema nchi inapita katika kipindi kigumu kutokana na dhuluma inayotendwa na watawala dhidi ya raia wasiokuwa na hatia.
“Huwezi kuamini kuwa dhuluma hii inatendwa na watawala Waislamu na hali ni mbaya, wananchi wanapata hilaki kubwa baada ya hao wanaojiita Serikali kubaini kuwa hawakubaliki.
Maalim Seif alieleza kusikitishwa na hali ya kamatakamata dhidi ya viongozi mbalimbali wa CUF katika ngazi za wilaya na majimbo na kuwekwa ndani huku wakiteswa, kuadhibiwa na kulazimishwa kukubali kushiriki katika vitendo vya uhalifu ambavyo hawakuvitenda.
“Hakuna haja ya kuwatesa watu, iwapo wanayo azma ya kunikamata, mimi nipo waje tu wanikamate,” amesema.
Maalim Seif alisema vitendo vyote hivyo ni mwendelezo wa dhuluma aliyoitenda Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha, tarehe 28 Oktoba 2015 wakati akifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kabla ya kuitisha ule wa marudio wa Machi 20.
Hii ni mara ya kwanza mpasuko wa kisiasa unawaathiri Wazanzibari hata wakati wa Sikukuu ya Eid -El Fitr inayoadhimishwa baada ya kumalizika mfungo ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

clouds stream