Friday 3 June 2016

Upinzani Wataja Sababu Sita Kumng’oa Naibu Spika

Naibu Spika wa Bunge Tulia Ackson.

Wabunge wa kambi rasmi ya upinzani wametoa sababu sita kwanini wanataka Naibu Spika Dk Tulia Ackson aondolewe madarakani kwa Azimio la Bunge baada ya kutangaza rasmi kususisa vikao vyote atavyoviendesha naibu huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya wabunge hao, Mbunge wa Simanjiro, James Millya (CHADEMA) alizitaja sababu hizo kuwa ni kwanza Dk Tulia ameweka maslahi ya chama chake cha siasa mbele kuliko maslahi ya Bunge, kinyume na Kanuni ya 8(b) ya Bunge.

“Pili, Mei 6 alitumia vibaya madaraka ya kiti cha Spika kwa kutoa uamuzi wa mwongozo ambao ulikuwa unakiuka Ibara ya 12(2) ya Katiba. Muongozo huo uliokuwa unapinga udhalilishaji wa wabunge wanawake,” alisema.

Ya tatu ni kitendo cha Dk Tulia kuvunja Kanuni ya 64(1) (f) na (g) zinazokataza mbunge kutumia lugha ya matusi kwa mbunge mwingine ambapo alinukuliwa akisema “Mheshimiwa Bwege, usionyeshe ubwege wako humu ndani.”

Alisema ya nne ni Mei 30 kiongozi huyo aliamua kwa makusudi kuvunja Ibara ya 63(2) ya Katiba na kutumia vibaya Kanuni ya 69(2) na 47(4) ya Kanuni za Bunge kumzuia Joshua Nassari kwa upande mmoja na Bunge zima kwa upande wa pili kutimiza majukumu yake ya kikatiba ya kusimamia na kuishauri Serikali.

“Sababu ya tano ni kuwa Mei 26, mwaka huu Dk Ackson akiongoza kikao cha Bunge bila ridhaa ya upinzani alishiriki kufuta sehemu ya hotuba ya msemaji wa upinzani kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kinyume cha kanuni ya 99(9) ya Bunge bila kushirikisha kamati yoyote ya Bunge,” alisema.

Sababu ya sita, Millya alisema kuwa ni kitendo cha Dk Ackson kukataa taarifa ya maoni tofauti, iliyowasilishwa na wabunge wanne wa upinzani.

Tangu Jumanne wiki hii wabunge hao wamekuwa wakisusa vikao vinavyoongozwa na kiongozi huyo kwa madai kuwa anaminya demokrasia.

clouds stream