Thursday 16 June 2016

Waziri Mkuu Azitaka Benki Kupitia Upya Viwango Vya Riba


Tarehe June 16, 2016majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka benki nchini zipitie upya riba zake ili watanzania waweze kukopa na kurejesha kwa urahisi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa Jumuiya ya Benki za Wananchi (COBAT) mjini Dodoma na kusema riba kubwa zinazotozwa na baadhi ya benki, huduma zisizokidhi mahitaji na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo wananchi wanapotaka huduma za kifedha.
Amesema changamoto nyingine ni kutokuwepo kwa taarifa mbalimbali za sheria na taratibu ambazo zinakwamisha ufanisi wa kiutendaji kwa baadhi ya taasisi hasa zile zinazolenga kuwahudumia watu wa kipato cha chini.
“Tunahitaji kutafuta njia bora ya kutatua changamoto hizi, na Benki za Wananchi ni kiungo muhimu katika kushughulikia changamoto zinazokabili utoaji wa huduma za kifedha,” amesema.
Waziri Mkuu amesema ni muhimu kuanzisha Benki za Wananchi katika kila Mkoa ili kuweza kusambaza huduma hizo karibu zaidi na walengwa, hali ambayo itasaidia kupunguza umasikini kupitia ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

clouds stream