Monday 27 June 2016

Wananchi Watinga Mahakamani Kudai Bunge ‘Live’



Tarehe June 28, 2016Bungeni-Dodoma
Katika hali isiyokuwa ya kawaida kundi la wananchi limetinga Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo kufungua kesi ya kuitaka mahakama hiyo kutengua agizo la serikali la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Kesi hiyo ina walalamikaji 10 ambao ni Azizi Himbuka, Perfect Mwasililwa, Rose Moshi, Penina Nkiya, Andrew Mandari, Hilda Sigara, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Mhe. Nape Nnauye pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaowakilishwa na mawakili Peter Kibatala na Omari Msemo wanaitaka mahakama kutengua uamuzi uliotolewa na Waziri Nape ambaye aliwasilisha kauli ya serikali bungeni juu ya uamuzi wa Serikali wa kutooneshwa moja kwa moja kwa vikao vinavyoendelea bungeni.
Walalamikaji wanaitaka mahakama itangaze kuwa, Raia wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wana haki ya kikatiba ya kujua majadiliano yanayoendelea bungeni kwa mujibu wa ibara ya 18(B), (d) na 29 (1).
Pili walalamikaji wamedai kuwa, serikali imekiuka haki ya kikatiba kwa kuzuia bila kuwa na sababu za msingi haki ya wananchi kusikia majadiliano ya Bunge kwa kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja.
Tatu, walalamikaji wameitaka mahakama kuilekeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurejesha haki ya kikatiba ya wananchi kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Nne, walalamikaji wamedai kuwa, matokeo ya kuzuia matangazo hayo ni kunyimwa kwa haki za Watanzania kutokana na kushindwa kuwasimamia pia kuwafuatilia wabunge na mwenendo wao bungeni.
Tano, walalamikaji hao wamedai kuwa, sababu za kuzuia matangazo hayo hazijitoshelezi hivyo Watanzania na walalamikaji wanayo haki ya kupata taarifa ya vikao vya Bunge  kwa maslahi ya taifa.
Hata hivyo upande wa utetezi ulidai kuwa, walichelewa kupata taarifa ya mashtaka hayo na hivyo hawakupata muda wa kutosha wa kuaandaa majibu. Kutokana na hivyo, mahakama iliuambia upande wa walalamikiwa kwamba, watajibu mashtaka hayo Julai 15, mwaka huu, siku ambayo kesi hiyo itatajwa tena.
Januari mwaka huu, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Mhe. Nape Nnauye alilieleza Bunge hatua ya Serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya chombo hicho kama ilivyokuwa awali.
Miongoni mwa sababu alizotoa ni kwamba, serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa gharama katika kuendesha matangazo hayo pia watumishi wa umma kutumia muda mwingi kuangalia Bunge badala ya kufanya kazi.
Hatua ya serikali kuzuia kurusha matangazo hayo ya moja kwa moja imeibua mjadala mkubwa kitaifa ambapo kada mbalimbali nchini zimekuwa zikipinga hatua hiyo.

clouds stream