Wednesday 21 January 2015

Yanga yatishia kujitoa ligi kuu ya vodacom.

Yanga yatishia kujitoa ligi kuu ya vodacom.


Mkuu wa Idara ya Habari a Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro.
Mkuu wa Idara ya Habari a Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro.
Mabingwa wa zamani wa ligi kuu ya Tanzania bara, Dar es Salaam Young Africans wametishia kutoingia uwanjani kucheza mechi yoyote ya Ligi Kuu ya Vodacom na michuano mingine, itakayochezeshwa ama kusimamiwa na waamuzi waliochezesha mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting wiki jana katika Uwanja wa Taifa.
Katika mtanange huo Yanga ilikuwa wenyeji wa Ruvu lakini mchezo huo uilitawaliwa na vurugu na kuisha kwa sare ya bao 0-0, huku nyota wa kimataifa wa Burundi, Amisi Tambwe akikabwa koo na kudhalilishwa na wachezaji wa timu hiyo ambayo inamilikiwa na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) mkoa wa Pwani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam katika Ofisi za makao makuu ya klabu hiyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amesema kuwa Yanga inayo ongozwa na Mwenyekiti Yusuf Manji, inalaani vurugu alizofanyiwa Tambwe na nyota wengine, huku wakitishia kutokuwa tayari kuchezeshwa na waamuzi hao.
Yanga imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutowapangia mechi zao za Ligi Kuu mwamuzi Mohammed Theofil wa Morogoro, wasaidizi wake Michael Mkongwa wa Njombe na Yusuf Sekile wa Ruvuma, pamoja na Kamisaa Kennedy Mapunda wa Dar es salaam.
“Tunaitaka TFF na Kamati ya Waamuzi, kuhakikisha hawawapangi waamuzi hao katika mechi zetu za Ligi Kuu na michuano mingine. Wakilazimisha kutupangia, tutakuwa tayari kugomea mechi husika na kupoteza pointi,”Amesema Muro.
Kutokana na vurugu zilizofanywa na nyota wa Ruvu Shooting kwa wachezaji wa Yanga, klabu hiyo imeitaka TFF kuanika hadharani ripoti ya waamuzi hao, ili wajiridhishe kuona kama wametendewa haki kwa kujumuisha matukio hayo kwenye ripoti hiyo, au la.
Ukiondoa maagizo hayo mawili, Yanga imetoa jumla ya mapendekezo manne, likiwamo la awali la kuitaka TFF kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika na vitendo vya ubaguzi na udhalilishaji, alivyofanyiwa Tambwe katika mchezo huo.
Pia, Yanga imetaka adhabu kwa mujibu wa sheria kutokana na kilichotokea katika mchezo huo, kuwafikia wote waliochangia kwa namna moja ama nyingine kukithiri kwa vurugu, ubabe, udhalilishaji na matusi, akiwamo beki aliyemkaba koo Tambwe, George Asei.
Kwa upande wake, Tambwe alisema amesikitika kwa lugha chafu, udhalilishaji, ubaguzi na vitendo vingine alivyofanyiwa katika mechi hiyo, ikiwemo kukabwa koo na kusema vitendo hivyo vikifumbiwa macho, vitachafua taswira ya soka la Tanzania nje ya nchi.

clouds stream