Monday 9 February 2015

Watu 6 kufariki kwa ajali ya moto, Rais Kikwete atuma salamu za rambirambi

Watu 6 kufariki kwa ajali ya moto, Rais Kikwete atuma salamu za rambirambi


RAIS Jakaya Kikwete.
RAIS Jakaya Kikwete.
Nyumba iliyoteketea kwa moto.
Nyumba iliyoteketea kwa moto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Saidi Meck Sadick kuomboleza vifo vya watu sita wa familia moja waliopoteza maisha kwa moto usiku wa kuamkia Jumamosi, Januari 7, 2015, katika eneo la Kipunguni A, Ukonga Banana, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha, katika salamu zake  Rais Kikwete amevielezea vifo hivyo kuwa ni vya kusikitisha na kuhuzunisha sana. “Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya vifo vya watu sita wa familia moja kutokana na kuunguzwa na moto.
Ni vifo vya kusikitisha na kuhuzunisha sana nakutumia wewe Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza pamoja nawe, ndugu na jamaa na wanaukonga wote msiba huu mkubwa na wa ghafla,” amesema Rais Kikwete na kuongeza.
“Naomba uniwakilishie salamu zangu na pole nyingi kwa wanafamilia, wanandugu na jamaa wote ambao wamepoteza wapendwa wao katika tukio hili. Wajulishe kuwa niko nao na naungana nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wetu hawa kwa sababu msiba huu ni wetu sote. Aidha, waambie kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aziweke pema roho za marehemu.”
Rais Kikwete ameongeza kuwa ni matarajio yake kuwa vyombo husika vya Serikali vitafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini chanzo na mazingira ya moto huo.

clouds stream